HABARI KUTOKA KWA CHANZO
Kwa mujibu wa chanzo makini, Uwoya alikumbana na tukio hilo hivi karibuni alipokwenda kwenye Mji wa Beni nchini Kongo kwa mwaliko wa kundi la wafanyabiashara waliotaka akawasimulie mashabiki wa marehemu Kanumba juu ya nini kilichotokea hadi staa huyo akafariki Aprili 7, mwaka huu na kuhitimisha msiba huo huko Kongo kwani kuna ambao bado walikuwa hawaamini habari za kifo chake.
WAPOKEWA NA UMATI
Ilielezwa kuwa baada ya kutimba nchini humo, Uwoya aliyeambatana na mwanamuziki ambaye pia ni mwigizaji, Patchou Mwamba ‘Tajiri’ na waigizaji Juma Chikoka na Mariam Ismail, walipokelewa na kushangazwa na umati uliokuwa umefurika ukumbini kutaka kumsikia mama Krish akisimulia kifo cha Kanumba.
UWOYA ALINDWA NA ASKARI SITA
Kabla ya kuanza kusimulia, Uwoya alielekezwa kila kitu ukumbini humo huku akilindwa na takribani askari 6 waliokuwa wamemwekea ulinzi mzito.
MZIMU WA KANUMBA
Madai nyuma ya pazia ni kwamba wakati Uwoya akisimulia tukio la kifo cha Kanumba, ghafla alimuona mtu kama marehemu Kanumba akiwa miongoni mwa wasikilizaji huku akiwa anamkazia macho hasa alipokuwa akizungumza mambo ya ndani ya marehemu, ndipo alipoishiwa nguvu ghafla, akadondoka na kuzimia.
Ilielezwa kuwa kitendo cha Uwoya kupata matatizo kiliibua vilio kwa mashabiki wa marehemu Kanumba lakini baadaye mwanadada huyo alirejea katika hali yake ya kawaida na kumalizia kusimulia tukio la kifo cha Kanumba.
HUYU HAPA UWOYA
Akizungumza na Risasi Mchanganyiko muda mfupi baada ya kutimba Dar, Juni 7, mwaka huu, Uwoya ambaye ni moto wa kuotea mbali kwenye filamu za Kibongo alifunguka kuwa wakati wanatia maguu Kongo walijua wanakwenda kumalizia msiba tu lakini kumbe wenyeji wao walikuwa wameandaa ukumbi ambao umefurika watu waliokuwa na shauku ya kujua kilichomuua Kanumba.
“Kusema kweli sikuwahi kufikiria kama ipo siku nitakusanya watu wengi kiasi kile ‘then’ nisimame mbele yao niwasimulie kifo cha Kanumba na mazishi yalikuwaje,” alisema Uwoya.
KUHUSU MZIMU WA KANUMBA
Akiendelea kusimulia, Uwoya alisema kuwa akiwa anasimulia kwa kujikaza huku akibubujikwa na machozi, alimuona mtu aliyekuwa na mavazi aliyovaa Kanumba kwenye filamu ya Magic House.
ASHINDWA KUVUMILIA, AZIMIA
Mbali na mavazi, Uwoya alisema mtu huyo alikuwa ameambatana na na watoto wawili wa kike na wa kiume waliovalia kama walivyovaa ‘wale watoto wa Kanumba’ kwenye filamu ya This is It hivyo kushindwa kuvumilia na kupoteza fahamu.
“Nilipoona vile, sikuweza tena kuongea, nilijishtukia nikiishiwa nguvu ghafla na kutaka kuanguka ila kwa kuwa kuna watu walikuwa pembeni yangu walinidaka na kunitoa eneo la tukio,” alisema Uwoya na kuongeza:
“Baadaye nilikuwa fiti na kumalizia kuwasimulia. Ukweli filamu zetu zinakubalika sana nchi za wenzetu.”
KWA NINI UWOYA?
Pamoja na Vincent Kigosi ‘Ray’, Uwoya alikuwa miongoni mwa waigizaji wakubwa wa Kibongo walioambatana na Kanumba mwaka jana kwenye uzinduzi wa filamu ya Off-Side nchini Kongo hivyo kujijengea jina kubwa pande hizo ndiyo maana wakamuita ili kusimulia kifo cha staa mwenzake.
Hizo zilikuwa ni Hisia zake tu,Kanumba is Dead na kamwe hatakuja kuonekana.