Timu
ya Taifa (Taifa Stars) imeagwa leo na kukabidhiwa bendera na Mkuu wa mkoa wa
Dar es salaam Mh. Said Meck Sadick tayari kuelekea nchini Msumbiji mapema kesho (june 15)kuikabili timu ya Taifa ya nchi
hiyo (The Mambas) katika mchezo wa marudiano wa kuwania kufuzu fainali za
mataifa ya Afrika utakaopigwa jumapili june 17.
Mkuu wa Mkoa (RC)
wa Dar es Salaam, Said Mecky Sadiki ameitaka timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa
Stars) kuiwakilisha vyema nchi katika mchezo huo. Ametoa
mwito huo leo (Juni 14 mwaka huu) wakati akimkabidhi nahodha wa timu hiyo Juma
Kaseja, Bendera ya Taifa tayari kwa safari ya kwenda Msumbiji itakayofanyika
kesho (Juni 15 mwaka huu) asubuhi. Stars itaondoka kwa ndege ya Kenya Airways
kupitia Nairobi.
Aidha RC
amesema kiwango ambacho kilioneshwa na Taifa Stars inayodhaminiwa na
Kilimanjaro Premium Lager kwenye mechi dhidi ya Ivory Coast na Gambia
kimerudisha imani ya Watanzania kwa timu hiyo, hivyo kuwataka wachezaji
kuendeleza moto huo.
Aliwataka
wachezaji wa timu hiyo pamoja na benchi la ufundi kupigana kiume kuhakikisha
wanashinda mechi hiyo, kwani ushindi mbali ya kuwaingiza katika raundi
inayofuata pia utaifanya Tanzania ipande kwenye orodha ya viwango vya ubora
duniani inayotolewa na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA).
Mechi
hiyo itakayochezeshwa na waamuzi kutoka Madagascar itafanyika kwenye Uwanja wa
Taifa ulioko Zampeto nje kidogo ya Jiji la Maputo kuanzia saa 9 kamili mchana
kwa saa za huko.
Waamuzi
hao ni Hamada Nampiandraza atakayepuliza filimbi, Alberto Razafitsatamy, Paulo
Andriovoavonjy na Bruno Andriamiharisoa. Kamishna wa mechi hiyo kutoka Botswana
ni David Fani.
Taifa
Stars inaondoka na msafara wa watu 32 wakiwemo wachezaji, benchi la ufundi na
viongozi. Msafara huo unaongozwa na mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Shaibu Nampunde.
0 comments for "Taifa Stars yakabidhiwa bendera tayari kuelekea Msumbiji"