Latest Stories

TOP 5 Most Popular Post

Recently Comments

FFFFFFFFFFFFF

FFFFFFFFFFFFF
XXXXXXXXXXX

FFFFFFFFFFFFF

FFFFFFFFFFFFF
XXXXXXXXXXX

Madaktari waomba ulinzi wa Dk. Ulimboka UN 0 Comments

By Unknown
Tuesday, July 10, 2012 | Posted in , ,

Kufuatia kuwepo kwa vitisho vya kutaka kukatisha maisha ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari nchini, Dk. Stephen Ulimboka, Chama Cha Madaktari Tanzania (MAT), kimeandika kwa Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa (UN) nchini kuomba ulinzi kwa daktari huyo.

Kwa mujibu wa barua hiyo yenye kumbukumbu namba MAT/UN/SU/01 iliyoandikwa Julai 7 na Rais wa MAT, Dk. Namala Mkopi kwenda UN, ilielezea mkasa mzima wa mgogoro uliopo baina ya serikali na madaktari nchini hadi Dk. Ulimboka alipofikwa na mkasa wa kutekwa na kupigwa na watu wasiojulikana.

Katika barua hiyo, Dk. Mkopi, alisema ofisa mmoja kutoka serikalini ameitaarifu MAT kwamba serikali imetuma maofisa usalama nchini Afrika Kusini anakotibiwa Dk. Ulimboka kwa ajili ya kuhakikisha kwamba harudi nchini akiwa hai.

Sehemu ya barua hiyo iliendelea kuwa "Mtu asiyefahamika kutoka Serikalini aliwaambia viongozi wa MAT kuwa watu kutoka Serikali ambao ni wauaji wametumwa kwenda Afrika ya Kusini kuhakikisha Dk. Ulimboka harudi nchini akiwa hai."

Barua hiyo iliendelea kueleza kuwa, mbali na hayo, viongozi wa MAT wamekuwa wakipigiwa simu za vitisho na kutumiwa ujumbe mfupi wa maneno (SMS) kupitia namba zisizofahamika.

Sehemu ya mwisho ya barua hiyo ilimalizia kwa kuiomba UN isaidie kumlinda Dk. Ulimboka hospitalini huko Afrika Kusini.

"MAT tunaiomba UN kuchukua jukumu la kulinda uhai wa Dk. Ulimboka hospitalini, kulinda usalama wa madaktari kutokana na vitisho wanavyopokea, pamoja na mhimili wa mahakama usikubali kuingiliwa kwa maslahi ya kisiasa," ilieleza sehemu ya barua hiyo.

Ilieleza kuwa madaktari walilazimika kumpeleka Dk. Ulimboka Afrika Kusini, kutokana na hali yake kuwa mbaya, kuhofia usalama wake na pia kupata tiba sahihi na uhakika.

Kadhalika, MAT imewaomba wataalamu wa kimataifa kuja nchini kusaidia kutatua mgogoro baina ya serikali na madaktari.

DK. MKOPI AITWA POLISI

Wakati huo huo, taarifa zilizopatikana kutoka kwa mmoja wa madaktari zilieleza kuwa Dk. Mkopi aliitwa kituo kikuu cha polisi majira ya mchana kwa mahojiano.

NIPASHE ilimtafuta Dk. Mkopi ili kujua sababu aliyoitiwa polisi na alisema Polisi walimwita kwa mahojiano kwa kumtuhumu kukiuka amri ya mahakama iliyotolewa Juni, 25 mwaka huu ya kusitisha mgomo wa madaktari.

Alisema mahojiano baina yake na polisi  yalianza saa sita mchana hadi saa 11 jioni, na kikubwa walikuwa wanamtuhumu kukiuka amri ya mahakama.

“Niliitwa na polisi majira ya saa sita mchana, kikubwa walichokuwa wananituhumu ni kushindwa kutii amri ya mahakama,’’ alisema Dk. Mkopi.

HALI YA DK. ULIMBOKA

Katika hatua nyingine, Katibu wa Jumuiya ya Madaktari, Dk. Edwin Chitage, anasema hali ya Dk. Ulimboka inaendelea vizuri na mpaka jana jioni hawajapata taarifa yoyote mbaya kutoka hospitalini.

Alisema wamepokea taarifa kuwa Dk. Ulimboka anaendelea vizuri na kwa sasa anaweza kula chakula mwenyewe.

SERIKALI YAFUTA POSHO ZA MADAKTARI 379

Wakati huo huo, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, imeeleza kusitisha posho za madaktari 379 walio katika mafunzo kwa vitendo katika hospitali mbalimbali nchini walioshiriki katika mgomo wa madaktari.

Taarifa ya Kaimu Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Regina Kikuli, kwa vyombo vya habari, alisema posho hizo zimesitishwa kuanzia Julai Mosi mwaka huu na kwamba madaktari wengine waliogoma, taratibu za kiutumishi zitachukuliwa na mamlaka ya ajira zao kwa mujibu wa sheria na taratibu husika.

“Kwa kuwa wizara ndio yenye dhamana ya usimamizi wa huduma za afya nchini, na kwa kuwa madaktari hao wamesajiliwa na Baraza la Madaktari Tanganyika, hivyo wizara imewasilisha malalamiko haya huko ili baraza liwachunguze na kuamua hatma yao kitaaluma,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

“Hivyo Wizara inasitisha posho zao kuanzia Julai 1, 2012 hadi hapo itakapopata taarifa ya uchunguzi wa Baraza  la  Madaktari,”  alisema Kikuli.

Alisema kuwa wameamua kuchukua uamuzi huo kutokana na kitendo walichofanya madaktari hao kilihatarisha usalama wa wagonjwa waliohitaji huduma za matibabu katika hospitali hizo, pia kilikuwa ni ukiukwaji wa maadili ya taaluma.

Madaktari hao ni kati ya 763 ambao wapo kwenye hospitali mbalimbali nchini wakifanya mafunzo kwa vitendo.

CHANZO: NIPASHE

Follow any responses to the RSS 2.0. Leave a response

Leave a reply

0 comments for "Madaktari waomba ulinzi wa Dk. Ulimboka UN"