Akijibu maswali ya waandishi wa habari baada ya kuwasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere, Dk. Migiro, alisema hana mawazo ya kuwania urais na hajui ni kwa nini watu wanazungumzia urais wakati bado rais aliyeko madarakani ana muda mrefu tu wa kuendelea kuwa madarakani.
Aliweka wazi kuwa kwa wadhifa aliopewa na Katibu Mkuu wa UN, Ban Ki-moon, kuwa mwakilishi maalum wa masuala ya ukimwi barani Afrika, kimsingi hataruhusiwa kushiriki katika siasa zozote za ndani ya nchi kwani sheria za UN ziko wazi.
Alisema mbali na kazi hiyo ya balozi wa ukimwi, pia anarejea kwenye kazi yake ya kufundisha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambako alieleza kuwa anaripoti leo kwa Mkuu wa Kitivo cha Sheria cha chuo hicho. Migiro alisema pia anataka kupata muda wa kukaa na familia yake kwani majukumu yake UN kwa miaka mitano yalimweka mbali kidogo, kwa hiyo kwa sasa ni fursa nzuri zaidi kukaa nayo.
Akiwa amefuatana na mumewe na binti yake, na kulakiwa na vigogo wazito wa mashirika ya Umoja wa Mataifa nchi, Unicef, Unaids, ILO na FAO wakiongozwa na Mwakilishi wa UN nchini, Alberic Kacou, pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Dk. Migiro pia alisema hana mpango wa kuwania nafasi yoyote ya uongozi ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi wa chama hicho unaoendelea.
Pia katika mapokezi hayo, walikuwako ndugu zake wengine na baadhi ya wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambako alifundisha kwa miaka mingi kabla ya kuingia kwenye siasa mwaka 2000 alipokuwa Mbunge wa viti maalum.
Balozi huyo wa Ukimwi Afrika, pia alisema anafurahi kuona kwamba Tanzania ni miongoni mwa nchi za Afrika ambayo imeamua kutengeneza Katiba mpya na kupongeza uamuzi uliofikiwa na Rais Jakaya Kikwete wa kuandikwa kwa katiba hiyo.
Aliwataka wananchi wote wajitokeze kutoa maoni yao juu ya Katiba wanayoitaka kwa kuwa ni fursa muhimu ya kuamua jinsi wanavyotaka kujitawala.
Akizungumzia mafanikio ya malengo ya milenia (MDG), alisema kwa ujumla Afrika imepiga hatua hasa katika eneo la elimu kwa kuwa idadi ya kuandikisha watoto wa kike sawa na wa kiume imeongezeka sana, na kusema kuwa changamoto iliyoko sasa ni usimamizi wake ili kuboresha huduma hiyo.
Alitoa mfano kuwa, njia mojawapo ya kuboresha elimu ni kupata walimu bora ili kuimarisha sekta hiyo.
Aliisifu Rwanda kama moja ya nchi za Afrika ambako hatua kubwa zimepigwa katika kufanikisha usawa wa kijinsia katika uongozi.
Hata hivyo, alisema bado umasikini ni changamoto kubwa katika kufanikisha MDG ingawa ana matumaini kwamba mafanikio makubwa yatafikiwa kwa bara la Afrika.
Kabla ya kuwa mbunge wa viti maaluma na kisha kuteuliwa kuwa Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto na baadaye Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na kuwa mwanamke wa Tanzania kushika wadhifa huo tangu uhuru mwaka 1961, mwaka 2007 aliteuliwa kushika wadhifa huo mkubwa ndani ya UN kabla ya kumaliza muda wake mwezi huu.
Dk. Migiro ambaye alikuwa mchangafu na aliyejawa na bashasha jana, aliwashukuru Watanzania na serikali ya Tanzania kwa ujumla kwa kumpa ushirikiano mkubwa wakati akitekeleza majukumu yake kama Naibu Katibu Mkuu wa UN kwa kipindi chake chote.
“Nawashukuru Watanzania kwani nafasi hii ilishikwa na Watanzania na Tanzania sehemu ndogo tu ya bara la Afrika” alisema.
Mwanadiplomasia huyo amekuwa anatajwa katika minong’ono mbalimbali nchini kuwa huenda akateuliwa na CCM kuwania urais mwaka 2015 wakati wa uchaguzi mkuu, wakati Rais Kikwete atakuwa anamaliza muhula wake wa pili na wa mwisho wa uongozi wake.
CHANZO:
NIPASHE
0 comments for "Dr. Asha Rose Migiro atua Dar, agusia mbio za urais 2015"