WAZIRI wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe, ameibuka ghafla katika Kituo
Kikuu cha Mabasi cha Ubungo (UBT), Dar es Salaam na kufanya ukaguzi wa nauli za
abiria wa kwenda mikoani na kusimamia waliolanguliwa kurejeshewa fedha.
Dk Mwakyembe aliyefika kituoni hapo jana saa 11.30 alfajiri na kuingia
katika mabasi, moja baada ya lingine, kukagua tiketi kwa abiria pia alisimamia
kutozwa faini kwa baadhi ya mabasi kuanzia Sh 250, 000 hadi Sh 750,000
kulingana na idadi ya makosa waliyokutwa nayo.
Pia aliwaagiza watendaji wakuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi
Kavu na Majini (SUMATRA), kufanya kazi ya ukaguzi kituoni hapo kwa miezi mitatu
mfululizo ili kuondoa matatizo yaliyopo.
“Nawataka sasa wote mwache kukaa ofisini, mtoke nje kufanya ukaguzi, muda
huu nilipaswa kuwa bungeni Dodoma, lakini kazi mliyopaswa kufanya nyie mimi
nawajibika kuifanya, kuanzia sasa nataka kuona kila mtu anafanya kazi yake
kikamilifu,” alisema Dk Mwakyembe.
Alianza ukaguzi huo kimyakimya katika basi la Green Star na kuendelea
katika basi la Musoma Express, huku akifuatana na Kaimu Mkurugenzi wa Sumatra,
Ahmad Kilima, watendaji wake na maofisa wa Polisi.
Udanganyifu nauli Katika ukaguzi huo aliofanya zaidi katika mabasi
yanayokwenda mikoa ya Mwanza, Mbeya, Musoma na Arusha, Mwakyembe alibaini
udanganyifu katika nauli ambapo abiria walikuwa wakitozwa kiasi kikubwa tofauti
na viwango vya Serikali.
Mabasi yaliyofanyiwa ukaguzi na kukutwa yakitoza nauli hizo ni Sumry,
Najimunisa, Musoma Express, ‘RS Bus’, Princess Shabaha, Buffalo na Best Line.
Mwakyembe aliyekuwa amesimama katika lango la kutokea mabasi kituoni
hapo, aliagiza kusimamishwa kwa kila basi lililokuwa likitoka na kuingia kuhoji
abiria nauli waliyotozwa kwa kila sehemu wanayokwenda, huku akitaka uthibitisho
kwa maofisa wa Sumatra aliokuwa nao.
“Tunashukuru Waziri kwa kuja kujionea hali halisi, ukweli sisi abiria
tunanyanyasika, wamiliki wengi wa mabasi haya wanapandisha nauli bila kufuata
utaratibu, ujio wako tunaamini utasaidia kuondoa tatizo hili,” alisikika abiria
ndani ya basi la RS, lililokuwa likienda Bukoba huku akiungwa mkono na wenzake.
Katika ukaguzi huo, Dk Mwakyembe alibaini kuwapo abiria waliotozwa Sh
60,000 kwa safari ya Bukoba tofauti na nauli halali ya Sh 51,000 katika basi la
hadhi ya anasa.
Wapo pia abiria wa Mwanza waliokutwa wametozwa nauli ya hadi Sh 45,000
kwa safari hiyo tofauti na Sh 35,000 ya Sumatra.
Abiria wa Singida, walitozwa nauli ya Sh 28,000 hadi Sh 38,000 wakati
halali ni Sh 21,000. Kukosa dereva wa ziada Mbali na masuala ya nauli, pia Dk Mwakyembe
alisimamia utozaji faini kwa mabasi yaliyobainika kuwa na dereva mmoja na
kusema yamekuwa chanzo cha ajali nyingi zinazosababishwa na uzembe wa madereva.
“Ajali nyingi zinazoendelea kutokea nchini kwa asilimia 75
zinasababishwa na uzembe wa madereva, hatutaki kuona maisha ya Watanzania
yakiendelea kupotea kwa uzembe huu,” alisema Dk Mwakyembe ambaye jana mchana
alitarajia kukutana na viongozi wa Sumatra na wadau wa sekta hiyo kwa ajili ya
mazungumzo.
Kaimu Mkurugenzi wa Sumatra, Ahmad Kilima, alisema sasa wanajipanga
kufanya kazi hiyo kwa nguvu zote, ili kubaini wamiliki wa mabasi wanaoendelea
kuvunja utaratibu wa usafirishaji kwa makusudi.
Alisema ufinyu wa wafanyakazi wa ofisi hiyo kwa kiwango kikubwa ndio
uliosababisha kufanyika kwa ukaguzi wa kusuasua, hivyo wanajipanga kuongeza
wafanyakazi ili kuimarisha ukaguzi.
Hatua ya Dk Mwakyembe kutembelea kituo hicho ni mwendelezo wa utaratibu
aliojiwekea tangu alipoteuliwa kushika nafasi hiyo na tayari amefanya ukaguzi
wa ghafla katika Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (Tazara), Shirika la
Reli (TRL) na Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL). Pia ni Waziri pekee ambaye hivi
karibuni alisafiri kwa treni Reli ya Kati kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma kuhudhuria
mkutano unaoendelea wa Bunge la Bajeti, ambapo pamoja na mambo mengine alikagua
ubora wa mabehewa na utendaji kazi.
0 comments for "Dk Mwakyembe 'avamia' mabasi Ubungo alfajiri"