KOCHA Mkuu wa timu ya Yanga Mbelgiji Tom Saintfiet,
ametangaza kikosi cha wachezaji 20 watakaocheza michuano ya Kombe la Kagame
huku nahodha wa timu hiyo Shadrack Nsajigwa akiwa miongoni mwa wachezaji
maarufu ambao hawataitumikia Yanga kwenye mashindano hayo.
Wachezaji wengine ambao kocha huyo amewaacha kwenye
kikosi chake ni kiungo mpya aliyesajiliwa Yanga hivi karibuni akitokea JKT
Ruvu, Frank Domayo na mshambuliaji chipukizi Simon Msuva kutoka Moro United na
viungo Omega Sema na Nurdin Bakari ambao walikuwepo Yanga msimu uliopita.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es
Salaam jana, Saintfiet alisema uamuzi huo umefikiwa baada ya kukaa na benchi
lake la ufundi na kwamba kazi kubwa imefanyika kuwapata wachezaji hao 20 kwani
kikosi chake chote ni kizuri.
Alisema anasikitika kwa wachezaji ambao hawapo kwenye
kikosi cha Kagame, maana wanahitajika 20 na hawakuwa na jinsi zaidi ya kufanya
vile ambavyo kanuni za mashindano zinataka.
Kuhusu Domayo, Msuva na Seme alisema bado ni vijana na
anaamini wataitumikia zaidi Yanga siku za usoni na kwamba ameamua kuwaacha ili
waelekeze nguvu zao katika timu ya Taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20
inayojiandaa kwa mashindano ya kimataifa, ambayo kwa sasa ipo kambini.
Kwa upande wa Nsajigwa alisema ni mchezaji muhimu sana
katika mashindano hayo, lakini anahitaji muda wa kupumzika kwa kuwa amecheza
mechi nyingi bila kupumzika kujiandaa na Ligi Kuu Tanzania Bara.
Kikosi kamili cha Yanga katika mashindano hayo
yanayoanza kesho kwa Yanga kucheza na Atletico ya Burundi ni Yaw Berko, Ally
Mustapha ‘Barthez’, mabeki ni Kelvin Yondani, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Juma
Abdul, Godfrey Taita, Oscar Joshua na Ladslaus Mbogo.
Viungo ni Stephano Mwasika, Athuman Idd ‘Chuji’,
Rashidi Gumbo, Juma Seif ‘Kijiko’, Haruna Niyonzima, Nizar Khalfan na Idrisa
Rashid, wakati washambuliaji ni Hamis Kiiza, Said Bahanuzi, Jeryson Tegete na
Shamte Ally.
Katika kikosi hicho pia hayupo mshambuliaji mpya wa
timu hiyo Meddie Kagere aliyetangazwa kusajiliwa akitokea Polisi ya Rwanda,
ambaye hata hivyo bado hajafika nchini.
Pia Tom amemjumuisha beki Kelvin Yondani aliyesajiliwa
akitokea Simba hivi karibuni ingawa usajili wake umekuwa na utata baada ya
Simba kudai bado ina mkataba naye.
Pia vyombo vya habari wiki hii vimeripoti kuwa Baraza
la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) ambalo
linasimamia mashindano hayo limeitaka Yanga imalizane kwanza na Simba kabla ya
kumtumia beki huyo.
Yanga ndiyo bingwa mtetezi wa mashindano hayo. Licha
ya kikosi hicho kocha huyo alizungumzia mchezo wa kesho na kusema utakuwa mgumu
lakini watapambana kwa vile wana ushirikiano wa kutosha na kuwaomba viongozi na
mashabiki wa Yanga kuachana na mawazo yaliyopita ya kufanya vibaya kwenye Ligi
Kuu na badala yake waelekeze mawazo yao kwenye Kombe la Kagame.
0 comments for "Nsajigwa, Domayo nje Yanga Kagame"