Waziri wa Ardhi,
Nyumba na Maendeleo ya Makazi Profesa Anna Tibaijuka amewasilisha bajeti ya
Wizara yake katika mkutano wa Bunge unaoendelea mjini Dodoma kwa kuzitaja
baadhi ya changamoto zinazoikabili Wizara hiyo kuwa ni pamoja na kuongezeka kwa
migogoro ya ardhi na nyumba katika maeneo ya mijini na vijijini.
Profesa Tibaijuka
amezitaja changamoto nyingine kuwa ni kukosekana kwa ardhi iliyopangwa na kupimwa
kwa ajili ya matumizi ya mbalimbali mijini na vijijini ikilinganishwa na
mahitaji pamoja na kuwepo kwa utamaduni ambao bado hauzingatii mfumo wa
ubananaji wa makazi ya mijini na kasi yake vinavyolazimisha kuheshimu sheria na
taratibu za mipango miji.
Aidha, Waziri wa Ardhi
alisema kubadilisha utunzaji wa kumbukumbu za sekta ya ardhi kutoka mfumo usio
unganishi kwenda kwenye mfumo unganishi wa ki-elektroniki ni miongoni mwa
changamoto zinazoikabili wizara yake.
Alisema changamoto
hizi zinakwamisha uendelezaji wa dhana halisi za upangaji, upimaji na utawala
wa ardhi na kuongeza kuwa ili kukabiliana na changamoto hizo, serikali kupitia
wizara hiyo itaendelea kujenga mfumo unganishi wa ki-elektroniki wa kuhifadhi
kumbukumbu za ardhi utakaowezesha upatikanaji na utumiaji wa kumbukumbu za
sekta ya ardhi kwa ufanisi.
Serikali pia itaandaa
mipango ya matumizi ya ardhi nchini hasa katika vijiji vilivyopo mipakani na
kuendelea kutekeleza programu ya Taifa ya kurasimisha na kuzuia makazi holela
mijini kwa kushirikiana na Halmashauri mbalimbali.
Alisema ili
kukabiliana na matatizo ya ardhi, wizara yake itaendelea kuimarisha vyombo vya
kusimamia maadili na weledi wa wataalam wa sekta ya ardhi katika ngazi zote na
kuandaa utaratibu utakaowezesha mamlaka za upangaji kuweka mfumo wa udhibiti na
uendelezaji wa ardhi katika ngazi ya kata.
Aidha Waziri huyo
alisema wizara yake itabuni mbinu mpya za kisasa ili kupata fedha za kuendeleza
shughuli za wizara nje ya bajeti kuu ya serikali na serikali za Mitaa hasa
kupitia mikopo ya benki au hisa za makazi.
Profesa Tibaijuka
ameliomba Bunge kuidhinisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara ya Ardhi,
Nyumba na Maendeleo ya Makazi ya shilingi 101,731,722,000. Kati ya fedha hizo,
shilingi 10,422,891,000 ni kwa ajili ya mishahara , shilingi 71,000,000,000 ni
miradi ya maendeleo na shilingi 20,308,831,000 ni kwa ajili ya matumizi
mengine.
0 comments for "WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI AWASILISHA BAJETI YA WIZARA YAKE BUNGENI"